Jukwaa la mijadala ya wazi la Café Talk limeendelea kuwa sehemu muhimu ya kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi na wadau wa uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Katika mjadala uliofanyika Mei 2, 2025, jijini Dar es Salaam, Wakili na Mshauri wa Kisheria Lwijiso Ndelwa alieleza umuhimu wa vyama vya siasa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Wakili Lwijiso amesema kuwa ingawa kanuni hazijasema moja kwa moja kuwa chama kisichosaini hakiwezi kushiriki, tafsiri ya kisheria inaonesha kuwa ushiriki wa chama hicho hautakuwa halali. Alisisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kusoma na kuelewa vizuri kanuni hizo ili kuepuka matatizo yatakayoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi.
Katika mchango wake, alifafanua kuwa vyama bado vina haki ya kuendelea na taratibu zao za ndani kama vile uteuzi wa wagombea, kwani kanuni hizo za maadili zitaanza kutumika rasmi siku moja baada ya Tume ya Uchaguzi kupitisha na kutangaza majina ya wagombea wa nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani.
Jukwaa la Café Talk limeelezwa kuwa mchango wake ni mkubwa katika kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria kwa wananchi, hasa wakati huu ambapo maandalizi ya uchaguzi yanaendelea. Mjadala huo ulihudhuriwa na wanasheria, wanahabari, na wadau mbalimbali kutoka sekta ya siasa na jamii.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mjadala huo, lengo kuu ni kutoa fursa kwa wananchi na vyama vya siasa kupata ufafanuzi kuhusu kanuni na miongozo ya Tume Huru ya Uchaguzi, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa misingi ya haki, uwazi na utawala wa sheria.