Wakili na Mshauri wa Kisheria Lwijiso Ndelwa amesema kuwa chama cha siasa ambacho hakitasaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani hakiwezi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Akizungumza Ijumaa, Mei 2, 2025, katika mjadala wa wazi wa “Cafe Talk” uliofanyika jijini Dar es Salaam, Wakili Lwijiso amefafanua kuwa ingawa kanuni hazijataja moja kwa moja kuwa chama hakiwezi kushiriki bila kusaini, masharti yaliyopo yanaashiria wazi kuwa ushiriki huo hautakuwa halali.
Amesisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kusoma kwa makini kanuni hizo ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza katika mchakato wa uchaguzi.
“Ni kweli kwamba kanuni hazijasema kwa maneno ya moja kwa moja, lakini kwa tafsiri ya kisheria, chama ambacho hakijasaini hakiwezi kuwa sehemu ya mchakato,” alisema Wakili Lwijiso mbele ya waandishi na wanasheria waliohudhuria.