TUICO: HAKUNA MGOMO WA WAFANYAKAZI SBC TANZANIA LIMITED




Na Mwandishi wetu 

Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimewataka Waajiri nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, na Miongozo mbalimbali inayoongoza Ulimwengu wa Kazi ili kuhakikisha haki, heshima na maslahi ya Wafanyakazi nchini vinastawi na kuondoa migogoro na mifarakano isiyo na tija.  

Hayo yamebainishwa katika Mkutano wa TUICO na Waandishi wa Habari uliofanyika Machi 31, 2022 jijini Dar es Salaam kufuatia habari iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Machi 23, 2022 iliyobebwa na Ndugu Said Ibrahim Stawi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa TUICO kiwanda cha SBC Tanzania Limited Dar es Salaam, aliyeibua suala la Ukiukwaji wa Sheria za Kazi katika kiwanda hicho.

Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TUICO, Wakili Noel Nchimbi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sheria amesema tarehe 28-03-2022 Ofisi ya Katibu Mkuu TUICO, Katibu wa TUICO Kanda ya Dar es Salaam, Uongozi wa SBC Tanzania Limited na Ofisi ya Kamishina wa Kazi Nchini walikaa Kikao cha Ndani kutafuta muafaka wa pamoja kuhusu changamoto zilizoibuliwa.

“Kutokana na Kikao hicho tayari kuna hatua ambazo zimeshaanza kuchukuliwa; na TUICO tutaendelea kutoa ushirikiano ili kutekelekeza makubaliano hayo ili haki, heshima, na maslahi vizidi kustawi na Wafanyakazi watambue wajibu, sambamba na kuheshimiwa kwa Mkataba wa Hali Bora za Kazi uliofungwa kati ya TUICO na SBC Tanzania Limited,” ameeleza Wakili Noel Nchimbi.

Katika hatua nyingine, Chama cha Wafanyakazi TUICO kimesema tuhuma zilizoibuliwa na Ndugu Said Ibrahim Sitawi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa TUICO katika Kiwanda hicho, siyo kauli ya TUICO bali ulikuwa utashi wa aliyezungumza. Kwa mujibu wa Katiba ya TUICO, Msemaji wa Chama ni Katibu Mkuu, na Chama bado kina mahusiano mazuri na SBC Tanzania Limited.

Chama cha TUICO kimesema kimeendelea na utoaji wa elimu kwa Wafanyakazi kuhusu Viwango vya Ajira hali ambayo imeongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya ajira sambamba na utendaji mzuri wa kazi hali inayofanya TUICO kuwa na Mikataba hai ya Hali Bora za Kazi zaidi ya 150 katika maeneo mbalimbali ya kazi ambayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri katika yake, Waajiri, na Serikali.

Aidha, TUICO kimetumia Mkutano huo kulaani vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa aina yoyote unaojitokeza kwenye maeneo mbalimbali ya kazi nchini na kusema kitaendelea kutoa elimu kwa Wanachama na Wafanyakazi kuhusu aina mbalimbali za unyanyasaji ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kingono ikiwa ni pamoja na kujenga mifumo rafiki ya kuripoti visa hivyo.

Mkutano huo umehudhuriwa na Ofisi ya Kamishina wa Kazi nchini, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Mwakilishi wa SBC Tanzania Limited, sambamba na Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.




Post a Comment

Previous Post Next Post