Tarehe
16 Novemba, 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ametoa
rai kwa Waajiri katika Taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinatekeleza
Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ili kulinda nguvu
kazi ya Taifa na kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Mhe. Simbawewene ametoa kauli hiyo
leo tarehe 16 Novemba, 2024 alipotembelea Wakala wa
Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) jijini Dar es Salaam kuhitimisha zoezi la
ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria katika usimamizi wa utumishi wa umma.
Mhe.
Simbachawene amesema Sheria hiyo ya Afya na Usalama
Mahali pa Kazi inaelekeza maeneo yote ya kazi nchini kuwa na Mifumo madhubuti
ya kuwakinga Wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwani
kinga ni bora kuliko tiba.
Ameongeza
kuwa, kwa kutambua umuhimu wa usalama na afya mahali pa kazi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilitunga Kanuni ya 105 ya
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 inayoelekeza Waajiri kuchukua
tahadhari zote dhidi ya ajali na magonjwa mahali pa kazi.
Ameipongeza
Menejimenti ya OSHA kwa kuendelea kuisimamia Sheria hiyo na kuhakikisha kuwa
Waajiri wanasimamia kikamilifu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili
kuwakinga watumishi wa Umma dhidi ya magonjwa, ajali na hata vifo.
Amesema kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998, Tume ya Utumishi wa Umma iliundwa ili kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unakuwa mmoja na watumishi wa umma wanakuwa na Taratibu za usimamizi wa utumishi wao unaofanana.
Hivyo, Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria katika
Usimamizi wa Utumishi wa Umma ni njia
mojawapo ambayo hutumika kupima ni kwa kiwango gani, Waajiri, Mamlaka za Ajira
na Mamlaka za Nidhamu wanazingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo
ya Utumishi wa Umma katika kusimamia Utumishi wa Umma.
Tume ya Utumishi wa Umma chini ya Kifungu cha
10(1(c) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, imepewa mamlaka ya
kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika usimamizi wa
Utumishi wa Umma ikiwemo usimamizi wa masuala ya Rasilimali Watu.
Akimkaribisha
Waziri Simbachawene kuzungumza na Menejimenti ya OSHA, Mwenyekiti wa Tume ya
Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji (Mst) Hamisa Kalombola amesema Tume imejiwekea
utaratibu wa Viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambao
ndio wasimamizi wa Tume hiyo kushiriki katika kuhitimisha zoezi la ukaguzi
uliofanyika kwa taasisi ili kushuhudia namna zoezi lilivyofanyika.
Akitoa
maelezo ya awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema ili nchi
iendee inahitaji nguvu kazi yenye afya, hivyo jukumu lao ni kuhakikisha
mifumo ya kulinda afya za watumishi
inawekwa katika taasisi za umma na binafsi ili kuzuia magonjwa yanayotokana na
kazi hayaathiri utendaji kazi wa watumishi
Kwa
upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama ameyataja
maeneo ambayo Tume imeyakagua kuwa ni ajira mpya, upandishaji vyeo, mafunzo na
maendeleo ya watumishi, nidhamu, likizo ya kustaafu na uzazi, uzingatiaji wa
maadili, ushughulikiaji wa mrejesho, usimamizi wa taratibu za ofisi ikiwemo
utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, anuai za jamii, mfumo jumuishi wa taarifa za
kiutumishi na mishahara, fidia ya ajali pamoja na magonjwa yanayotokana na
kazi.