Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amedai vurugu zilizojitokeza juzi wakati wa uchaguzi wa kutafuta viongozi wa chama Mkoa wa Arusha zilichochewa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila.
Lema ameyabainisha hayo leo Novemba 16,2024 wakati akizungumza na wanahabari jijini Arusha.
"Hii ilikuwa ni organised crime kati ya watu wa CHADEMA na ndiyo maana na ninyi waandishi wa habari mlipatikana.Cha kusikitisha zaidi na hii ninaogopa kusema kwa sababu ninalisema, lakini ninaumia sana.
"Cha kusikitisha zaidi yale mambo mimi nilimuomba Naibu Katibu Mkuu Bara ateremke,Bw.Benson Kigaila...ateremke na nilimuomba ateremke awazuie wale wafanya fujo kwa sababu mmoja wa wafanya fujo ni rafiki yake mkubwa.
"Ambaye siku chache zilizopita alifanya fujo Monduli, mmoja wa wafanya fujo na alipofanya fujo Monduli mpaka uchaguzi wakamtukana msimamizi.
"Halafu wakati wakifanya fujo Monduli, mimi nilishuhudia kwamba, msimamizi alinipigia simu, nikamwabia afadhali hapa nipo na msimamizi wa uchaguzi Bw.Benson Kigaila unaweza ukaongea naye akasema hawa wanataka kunipiga.
"Wamepora na matokeo ya mabaraza,sasa sijui waliongea nini, lakini alisema kama uchaguzi wa wilaya haujatimia funga, halafu watu wa hamasa wakuondoe hapo muondoke.
"Kesho yake, mimi nikiwa na Benson Kigaila mmoja wa wafanya fujo akampigia simu, akaongea nae kama dakika 20.
"Niko na Benson, Moshi nikamwambia Benson, Naibu Katibu Mkuu Bara hawa watu wamefanya fujo, wamedhalilisha watu.
"Unapowapa audience ya kuongea nao na unapokuwa submissive kwao, alikuwa akiongea naye yeye akionekana kuwa mnyenyekevu kwao.
"Unatunyima sisi wengine mamlaka ya kichama, nikamwambia hii sio sawa sawa.
"Nikamwambia the ways unavyoongea na huyu Bwana hauongei sawa ni rafiki yake sana, Boni ni rafiki yake sana Benson Kigaila.
"Benson Kigaila akija hapa, anafikia kwa Boni na wakati mwingine wanatembea kwa pamoja, wanakula pamoja
"Ni rafiki sana na Naibu Katibu Mkuu Bara, huyu aliyekuwa anatukana sana, lakini kinachonishangaza sana ni kwamba hata yule wa Ngorongoro aliyekuwa anatukana akisema kwamba... mimi nimekata majina yao.
"Sasa, hili jambo nitalisema kwamba mimi kwenye usaili huu maamuzi yoyote yakifanyika yanafanyika with collective responsibility.
"Lakini, mtu aliyeleta taarifa za Kuyaa, za tabia zake mbaya huko Ngorongoro, mbaya sana ni Naibu Katibu Mkuu Bara na akashawishi wajumbe kwamba huyu mtu hana sifa za kuwa kiongozi,"amedai Lema.
Hata hivyo, Lema amedai tayari ameagiza wote waliofanya fujo wachukuliwe hatua.
"Lakini, msimamo wa kwanza nimeagiza viongozi wa chama kanda mahali popote, kwa yeyote aliyehusika kwa sababu wako waliotoka Mkoa wa Kilimanjaro walikuja kufanya fujo Arusha.
"Kwamba taarifa ziende na wameziona hawa wanachama waliofanya huo upumbavu wa kiwango kile na kusababisha taharuki kubwa na udhalilishaji kwa chama chetu.
"Wachukuliwe hatua mara moja za kuvuliwa uanachama katika matawi yao mara moja na haraka iwezekanavyo,kwa sababu wamekidhalilisha chama sana,"ameongeza Lema.