Watanzania wametakiwa kuendelea kupanda miti ili kutunza mazingira ikiwemo kunyonya hewa ya ukaa na kuzalisha hewa safi ili kwenda sambamba na mpango wa Serikali wa upandaji wa miti kuzuia athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya mashariki kusini Bw. Hamadi Taimur Kissiwa ambaye alimuwakilisha Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais muungano na mazingira Dkt. Selemani Jafo wakati wa kuzindua na kuendeleza kampeni ya SOMA NA MTI katika shule ya msingi Buguruni Viziwi Jijini Dar es salaam leo Jumatatu Januari 30, 2023
Kampeni ya upandaji wa miti kwa wanafunzi wa shule inayofahamika kama ‘Soma na Mti’, ilizinduliwa rasmi jijini Dodoma Januari 20, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo kwa lengo kuwafanya wanafunzi waone zoezi la upandaji miti sehemu ya maisha ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza baada ya kuzindua kampeni hiyo shuleni hapo Meneja Kissiwa amesma kuwa maana ya soma na mti ni kwamba mtoto anatakiwa apande mti, akue nao hadi kipindi anaondoka shule mti aliopanda utakua umekua .
Pia ameupongeza wakala wa misitu Tanzania kwa kampeni ya ' Kata Mti manda Miti' ambapo amesema kuwa kampeni hiyo imesaidia kupunguza ukataji wa miti kiholela kwasababu hata kama mtu amepanda mti nyumbani kwake lazima aombe kibali kama anataka kukata mti.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Buguruni Viziwi Bwa. Yahaya Maftaa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa karibu na shule zenye uhitaji maalum huku akimshukuru waziri Jafo kwa kuweza kuiona shule ya Buguruni Viziwi kutekeleza kampeni ya SOMA NA MTI.