Tanzania na Iran kujenga chuo kikuu cha Kiswahili.




Na John Mapepele

Tanzania na Iran zimekubaliana kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili nchini ikiwa ni mkakati wa kuimarisha  mahusiano mazuri katika eneo la utamaduni baina ya nchi hizo.

Makubalino hayo yamefikiwa  Septemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam katika kikao baina ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa  na ujumbe kutoka  Chuo Kikuu cha Kimataifa cha  Al- Mustafa  Iran ulioongozwa na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mhe. Hossein Alvandi Bahineh.



Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa  Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu hicho ambacho  kitasaidia kubidhaisha lugha adhimu ya Kiswahili duniani kwa kupata wanafunzi  kutoka nchi mbalimbali duniani.

Amesema  kutokana na umuhimu wa lugha  hiyo Shirika la Utamaduni duniani ( UNESCO) limeipitisha  lugha hiyo kuwa ni miongoni mwa lugha itakayokuwa ikitimika katika mikutano ya kimataifa.

Aidha, amesema  kwa sasa lugha hiyo inatumiwa na zaidi ya watu milioni 250 duniani kote na kufundishwa kwenye vyuo vikuu maarufu duniani.



Amesema kwa sasa  wanasubiri kutiliana saini makubalino hayo baada ya kila pande kupitia mikataba hiyo katika kipindi kifupi kijacho.


Ameongeza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri wa tamaduni nzuri ambazo zimeota mizizi kutokana na  usimamizi thabiti kuanzia kuasisiwa taifa hili  na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na  Marais  wote hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mageuzi makubwa kwenye lugha hiyo hadi kutambulika kuwa lugha rasmi kimataifa na kupewa siku maalum ya kuiadhimisha ambayo ni Julai 7, ya kila mwaka.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na UNESCO katika kuhakikisha  Kiswahili kinabidhaishwa na kutumia duniani kote.

Rais wa Chuo hicho, amesema kwa sasa Chuo tayari kinafundisha  lugha za kimataifa 17 za nchi mbalimbali duniani ambapo pia baada ya kukamilika ujenzi  wake lugha nyingine zitafundishwa.

Aidha, ametoa wito kwa wataalam  wa Tanzania kwenda Iran kwa ajili ya kujifunza na kubadilisha  uzoefu katika  eneo  la utamaduni.


Post a Comment

Previous Post Next Post