Serikali kuzindua mikopo isiyo na riba kwa wasanii - Mhe. Mchengerwa




Na John Mapepele

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inakwenda kufanya uzinduzi wa utoaji wa mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni  ndani ya siku kumi kutoka sasa ili wasanii waweze kunufaika na mfuko huo ambao Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeuanzisha kuwanufaisha wasanii.


Hayo yamesemwa  leo Septemba 7, 2022 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa baada ya kikao na Watendaji wa Benki ya CRDB, Benki ambayo itatumika kwa ajili kutoa mikopo hiyo kwa niaba ya Serikali.



Mhe. Mchengerwa amesema  uzinduzi huo utafanywa  ndani ya siku kumi kuanzia sasa ambapo amefafanua kuwa mikopo hiyo haitakuwa na riba yoyote ili wasanii wengi waweze kunufaika mikopo hiyo.

Amesema  katika  tukio la uzinduzi wa mikopo hiyo  pia  Muongozo wa Uendeshaji  Mfuko utazinduliwa  ili vigezo na masharti ya uombaji wa mikopo vieleweke kwa  waombaji.


Aidha,  amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Samia Suluhu Hassan ilianzisha Mfuko huo  kwa lengo la utoaji wa mikopo, mafunzo na ruzuku kwa wananchi wanaojishughulisha  na utengenezaji, uzalishaji na uwekezaji wa miundombinu ya Utamaduni na Sanaa pamoja  na kuinua  vipaji na kuzalisha kazi  za ubunifu zenye kukidhi viwango vya soko la kitaifa.

Waziri Mchengerwa ametaja  baadhi ya walengwa  wa mfuko huo ni pamoja na watu binafsi wanaojishughulisha  na kazi za Sanaa, utamaduni waliosajiliwa katika  mamlaka za Serikali zinazosimamia  kazi za Utamaduni na Sanaa na vikundi vya Utamaduni na Sanaa. 

Wengine ni vyama vya Utamaduni na Sanaa, Mashirikisho ya Utamaduni na Sanaa, asasi  za kiraia zinazojishughulisha  na masuala  ya Utamaduni na Sanaa pamoja na vituo vya elimu na mafunzo  yanayohusiana na Utamaduni na Sanaa.


Amefafanua kuwa dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuwainua  wasanii na wadau mbalimbali wanaojishughulisha Sanaa na Utamaduni ili waweze kutengeneza kazi bora zitakazoweza kuuzwa katika  masoko ya kimataifa na kuinua uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post