Na John Mapepele, Arusha
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameibuka miongoni mwa wachezaji waliong'aa katika mechi ya kihistoria baina ya marais wa mashirikisho ya soka wa mataifa ya Afrika na wachezaji nguli duniani leo Agosti 10, 2022 jijini Arusha.
Mechi hiyo imechezwa jioni ya leo katika eneo la Shule ya St. Constantino baada ya kumalizika mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika( CAF) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha na kuhudhuriwa na wageni kutoka nchi 58 duniani.
Katika mechi hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa aliifungia timu yake goli baada ya kuwachanganya mabeki wa timu pinzani.
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo Mhe. Mchengerwa alitoa zawadi za Serikali kwa viongozi mbalimbali wa FIFA na CAF.
Miongoni mwa viongozi hao ni Rais wa FIFA Gianni Infantino, Rais wa CAF Patrice Motsepe na Katibu Mkuu wa CAF.
Mhe. Mchengerwa amesema haya ni mafanikio makubwa kwa Tanzania kuandaa mkutano huo ambao umekwenda kuitangaza Tanzania kimataifa.
Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kutumia michezo kuitangaza Tanzania kimataifa.
Tags:
HABARI