Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dodoma, Salum Ismaili Salum, ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini, mkoani Shinyanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Salum amesema ameamua kuingia katika kinyang’anyiro hicho kufuatia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kutoa fursa kwa vijana kushiriki katika uongozi wa nchi.
Salum ameeleza kuwa dhamira yake ya kugombea ubunge ni kuwaletea maendeleo wananchi wa Kahama Mjini, akitaja rasilimali zilizopo jimboni humo, ikiwemo migodi ya madini, kuwa ni fursa kubwa ya kuinua uchumi wa wananchi ikiwa zitasimamiwa vyema.
Amesema kuwa anatarajia kuchukua fomu ya kugombea ubunge tarehe 28 Juni 2025, na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kuchangamkia nafasi za uongozi kwa ajili ya kulijenga taifa.
Katika hatua nyingine, Salum amewakemea baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanaochochea uvunjifu wa amani nchini, akisisitiza kuwa hatowavumilia watu wa aina hiyo na kwamba ni lazima wadhibitiwe ili kulinda umoja na mshikamano wa taifa.
Aidha, amewasihi Watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Samia kutokana na juhudi na mafanikio makubwa aliyoyapata tangu alipochukua madaraka kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe Magufuli.
“Wakati Rais Samia anaingia madarakani, kulikuwa na mashaka kutoka kwa baadhi ya watu wakidhani kuwa hatoweza kuendeleza miradi ya maendeleo. Lakini ameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi kwa kuikamilisha na kuanzisha mingine mipya, jambo ambalo linaendelea kuwavutia na kuwahamasisha Watanzania wengi kumuunga mkono,” alisema Salum.
Ametoa wito kwa wananchi kuwapuuza watu wanaomkosoa na kumdhalilisha Rais Samia, akisisitiza kuwa ni muhimu kudumisha heshima kwa viongozi na kulinda amani ya taifa.