Mlinzi shule ya sekondari Marungu achukuliwe hatua



Na Hadija Bagasha Tanga,

Baraza la madiwani la Halmashauri ya jiji la Tanga  limelitaka jeshi la polisi Wilaya ya Tanga kumchukulia hatua za kisheria  mlinzi aliyekuwa akilinda kwenye shule ya Sekondari Marungu  ambaye anadaiwa kusababisha moto uliounguza jengo la ofisi ya utawala ambapo nyaraka na vyeti mbalimbali vimeteketea kwa moto. 

Taarifa za awali zilizopatikana zinaeleza kwamba mlinzi huyo anadaiwa kuchoma moto jengo hilo akiwa katika harakati za kufukuza nyuki ambao walitanda katika eneo hilo la shule kulingana na maelezo ya mlinzi huyo moto huo ulizuka gafla katika shule hiyo na kuenea hadi katika jengo hilo la utawala ambapo ulichoma nyaraka muhimu na vyeti vilivyokuwa vimehifadhiwa katika jengo hilo. 

Baraza hilo limeagiza kumkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria mlinzi wa shule hiyo ili upelelezi uendelee na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. 

Akitoa taarifa katika kikao cha baraza la madiwani  cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 Mstahiki Meya wa jiji hilo Abdulrahman Shiloo amesema kuwa baraza hilo halijaridhishwa na matokeo  ya taarifa  za upelelezi zilizofanywa na ofisi hiyo.

Taarifa za awali za kuungua kwa jengo hilo zilieleza kuwa aliyewasha moto katika jengo hilo ni mlinzi ambaye aliona nyuki wakiwa ndani ya ofisi hiyo na hivyo kuamua  kuchukuwa hatua hiyo ya kuwasha moto huo. 

"Jengo lile lilikuwa na vyeti nyaraka na taarifa zote za ujenzi wa maabara  inaonekana kwamba pale pana hujuma iliyofanyika  kwahiyo baraza la jiji la Tanga halijaridhika na  maelezo ya upelelezi yaliyotolewa na ofisi ya  upelelezi ya jeshi la polisi wilaya ya Tanga tunataka upelelezi huo uendelee na hatua za kisheria ziendelee na zichukuliwe kwa mlinzi yule kwa kupelekwa mahakamani" alisema Shiloo.

Awali Mstahiki Meya huyo alizungumzia kuhusu taarifa za hujuma zinazofanywa na baadhi ya watumishi waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia miradi ya ujenzi hasa ya madarasa ambapo ameeleza kwamba kuna mahali pamejengwa darasa linalodaiwa kugharimu milioni 20 lakini halina samani ndani yake  na  hivyo ameonya jambo hilo na kusema uongozi wa Halmashauri hautafumbia macho jambo hilo. 

Katika kikao hicho baraza hilo limeazimia kujenga shule ya sekondari katika kata ya Makorora yenye majengo ya gorofa kulingana na ufinyu wa eneo husika  kabla ya 2025 kata hiyo iwe na shule ya sekondari na hivyo kuhitimisha lengo la Halmashauri ya jiji la Tanga kuwa kila kata angalau iwe na shule moja ya sekondari. 

Hata hivyo kwenye kikao hicho Mstahiki Meya alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo Dkt. Spora Liana kwenda kuvunja nyumba ya mwananchi mmoja ambaye amejenga ndani ya eneo la barabara inayotoka Ikulu ndogo ya Tanga kwa sababu mwenye kiwanja hicho tayari ameshakabidhiwa kiwanja kingine ili aweze kujenga nyumba katika eneo jingine. 

Katika kikao hicho diwani mteule wa Kata ya Mnyanjani Simba Kayaga ameapishwa ambaye anayechukua nafasi ya marehemu Yakub Nour aliyefariki mwishoni mwa mwaka jana. 



Post a Comment

Previous Post Next Post