Viongozi wanaokwepa kulipa kodi wapewa onyo



Na Hadija Bagasha Tanga, 

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulah amewaonya baadhi ya viongozi wanaokwepa kulipa kodi za mapato katika biashara zao kwa vivuli vya vyeo walivyonavyo na badala yake wametakiwa kuacha mara moja tabia hiyo kwani imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya wananchi. 

Pia amewataka wafanyabiashara wote ambao ni viongozi na wanapswa kulipa kodi kuhakikisha wanafanya hivyo na kuziagiza mamlaka zinazoshughulikia na usimamizi wa kodi kutowafumbia macho viongozi hao na iwapo watakaidi watoe taarifa kwa ngazi husika. 


Kufuatia hatua hiyo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba kusimamia mapato ya Mkoa wa Tanga kwenye ukusanyaji wa mapato kwani ndio kigezo kikubwa cha mafanikio ya Mkoa  huo. 

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar ametoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye ziara yake Wilayani Lushoto kwenye jimbo la Mlalo kata ya Mtae Mkoani Tanga. 

Amesema changamoto ya ukusanyaji mdogo wa mapato katika baadhi ya maeneo nchini yanatokana na baadhi ya viongozi kutumia dhamana ya vyeo vyao kutolipa mapato ya serikali jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya wananchi. 

"Haya ni magumu kuyasema maana, kwenye maeneo mengine inakuwaga shida sana na  hii si huku bara tu hata kule kwetu Zanzibar eneo la makusanyo linakuwa na shida kwasababu viongozi sisi tunajaribu kujimilikisha wewe una duka lako hutaki kulipa unaacha kwasababu wewe ni diwani hiki kitu hakikubaliki kabisa, "alisema Abdulah. 


"Suala la kulipa kodi hili halina mjadala hili halina Mwenyekiti,  Mbunge,  diwani sio tu kuwaachia wananchi wenyewe kwani watu wote ni lazima walipe kodi ipasavyo, "Aliongeza kuwa

"Waheshimiwa wakuu wa wilaya mko hapa,  wakurugenzi mko hapa waheshimiwa, madiwani mko hapa nyinyi ndio watu wa kwanza mnaotakiwa msimamie mapato kwenye maeneo yenu ili wananchi hawa waweze kutatuliwa changamoto mbalimbali zinazowakabili, "alisisitiza Abdulah

Alisema kitendo cha kukataa kulipa kodi ni kuwaumiza wananchi ambao ndio wapiga kura wa chama cha mapinduzi ccm na hivyo ameagiza mtu yeyote asionewe katika suala hilo ni vyema kila mmoja atimize wajibu wake. 

"Ukiona kuna mtu anang'ang'ania mapato ya serikali hataki kutoa kwasababu ya cheo chake basi hafai kuwa kiongozi kwakuwa anakwenda kinyume na kiapo chake kwani kuna, kipengele kinasema cheo ni dhamana na hakitatumika kwa maslahi ya mtu binafsi niwaombe sana sijapata taarifa hiyo hapa lakini niwaombe sana jambo hili huwa ninalisema kila ninapokwenda ili tuwe tunazungumza lugha moja na sote tuwe na huruma na wananchi wetu, "alibainisha Makamu. 


Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mlalo Rashid Shangazi amemsukuru Makamu wa pili wa Rais kwa kufika jimboni humo kwani ameweka historia ya kuwa kiongozi wa pili kufika eneo hilo la Mtae. 

Mbunge Shangazi amemshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea maendeleo wananchi wake na kueleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano hadi 6 tarafa hiyo haikuwa na kituo cha polisi ambacho hivi saaa kipo,  haikuwa na mahakama kwani mahakama iliyokuwepo hapo awali ilijengwa na wakoloni mwaka 1920 pamoja na ujenzi, wa kituo cha afya kinachokwenda kuhudumia takribani kata 5 za kata ya Mtae ambapo hapo awali kulikuwa na kituo kimoja pekee. 

"Wananchi wa hapa walikuwa wanapata shida sana na vifo vya mama na mtoto kweni wengi walikuwa wanatoka tarafa ya Mtae hadi wilayani Lushoto ambacho kipo zaidi ya kilomita 60 kutoka eneo hilo, "alisema Mbunge Shangazi. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Omari Mgumba amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea na mipango ya kuufungua Mkoa Tanga katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii hususani katika hifadhi ya Mkomazi. 

Hifadhi kubwa ya Mkomazi zaidi ya asilimia 60 ipo Mkoa wa Tanga na asilimia 40 pekee ndio ipo Mkoani  Kilimanjaro tunamshukuru Rais kwa nia yake njema ya kutaka kuufungua utalii ndani ya Mkoa Tanga na Tanzania kwa ujumla nia ya kuanza ujenzi wa geti hili la kuingia Tanga pale Kamakota ambalo lipo kilomita 13 hivyo ombi letu tunafahamu mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo ilikuwa lijengwe tangu mwaka 2021 lakini kutokana na changamoto za Covid limechelewa kuanza, "alisema Mgumba

"Nikuombe kama mlezi jambo hili tayari limeshapita kwenye bajeti sisi tutasukuma kwa nafasi yetu kama serikali lakini na wewe tunaomba utusemee ndani ya chama sababu wewe unaingia ndani ya vikao vingine vikubwa ambavyo mimi siingii ombi letu ni kwamba geti hili lijengwe haraka iwezekanavyo ili likafungue utalii na kuendelea kumuunga mkono Daktari Samia kwenye kufungua utalii Tanga na Taifa kwa ujuma, "alisisitiza Mgumba. 

Wananchi wa eneo hilo la Mtae wanajishughulisha na shughuli za kilimo na hasa kilimo cha mazao ya viungo ikiwemo Tangawizi,  Iliki, na Mdalasini.


Post a Comment

Previous Post Next Post