BENKI YA TCB YAENDELEA KUTOA FURSA YA MIKOPO KWA WASTAAFU


Na Mwandishi wetu 


Benki ya TCB imeendelea kutoa fursa kwa wastaafu kwa kuwapa mikopo iliyo nafuu pamoja na kutoa elimu ya   namna ya kutumia fedha wanayoipata baada ya kustaafu

Hayo aliyasema Mkuu wa Kitengo cha Wastaafu kutoka Benki ya TCB, Haika Mbaga wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jana katika kufunga semina maalum kwaajili ya wastaafu zaidi ya 5000 iliyoanza mwezi Machi, 2022 katika mikoa yote na baadhi ya Wilaya. 

"Tunaleta semina hizi kwa wastaafu kwasababu sisi tumehudumia wastaafu kwa muda mrefu na tuna uzoefu mkubwa hivyo tunatambua mahitaji yao, wastaafu wanahitaji mengi hata baada ya kustaafu na hitaji moja wapo ni kuweza kujua wanawezaje kujikwamua kimaisha hata baada ya kustaafu kwasababu wengi wanapata sintofahamu nawezaje kupiga hatua mpya baada ya kustaafu"



Aidha Mbaga alisema mpaka sasa zaidi ya wastaafu 60,000 wamenufaika na mikopo hiyo ambayo imewawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kujikwamua kimatibabu.

"Benki yetu inatoa fursa nyingi sana kwa wastaafu, tunatoa mikopo kwa wastaafu na tunauzoefu mkubwa na wastaafu zaidi ya 60,000 wameweza kunufaika na mikopo hii nchi nzima, hilo ni kundi kubwa sana la wastaafu hivyo katika fursa hizi za mikopo wastaafu wameweza kunufaika na mikopo mingi kwa kusomesha watoto na wajukuu, kufanya shughuli za kiuchumi na kuongeza uchumi wao na kwenda kwenye sehemu tofauti tofauti katika kujikwamua kimatibabu"


Pia Mbaga alisema Watu wengi wanawatumia wastaafu kuwatapeli na kuwadanganya hivyo wao kama Taasisi ya fedha wapo kuwaonesha muelekeo kama wazoefu katika sekta ya fedha.

Mbali na hayo Mbaga alisema katika kuendelea kuwanufaisha,  kuwathamini na kuhakikisha mstaafu na Benki ya TCB wapo pamoja, wamekuja na akaunti maalumu kwa wastaafu hao iitwayo KIVULINI ambayo ina gharama za chini isiyo na makato makubwa na kumfanya mstaafu kuweza kukata bure na kupewa ATM Card bure.


Mbaga alisema tangu mwaka 2014 Benki ya TCB ndiyo ilikuwa benki ya kwanza nchini Tanzania kuleta fursa kwa wastaafu, kundi kutokana na kwamba kundi hilo kusahaulika katika fursa za taasisi za fedha na ambapo tangu mwaka huo mpaka sasa wameweza kuwahudumia wastaafu kwa idadi kubwa zaidi.

Kwa upande wake Mstaafu wa Benki ya TCB Ayoub Athumani, , alisema Semina hizi kutoka Benki ya TCB zinawanufaisha kwasababu zinawafundisha jinsi ya matumizi ya wastaafu pale wanapopata fedha jinsi ya kuweza kuzitumia hivyo amewashauri wastaafu wenzake wachukue fursa hiyo ya semina ili waweze kujiwekea malengo yao ya kuweza kujinufaisha katika kipato atakachokipata ili aweze kutumia vyema katika matumizi yake ya kawaida.


Naye Mariam Kambi,ambaye ni mstaafu aliwashauri wastaafu wote kutotumia vibaya pesa zao, watumie kwa utaratibu, waweze kuendesha maisha yao.

Simioni ambaye ni mstaafu kutoka manispaa ya Temeke alisema mbali na kusaidiwa kupata mikopo ambayo inawasaidia kuanzisha biashara mbalimbali aliiomba serikali kuongeza kiwango cha wastaafu ambacho kimebaki kwa muda mrefu.

Post a Comment

Previous Post Next Post