Na John Mapepele, Arusha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi,leo Agosti 10, 2022 ameuongoza ujumbe wa juu wa Shirikisho la soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kupanda miti ya matunda jijini Arusha.
Dkt. Abbasi amewaongoza Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Dkt. Patrice Motsepe wa CAF katika eneo la Shule ya St. Constantino, Arusha, kabla ya mechi ya kirafiki ya viongozi hao iliyochezwa jioni ya leo Agosti 10, 2022.
Mechi hiyo iliwashirikisha marais wa mashirikisho ya soka katika nchi za Afrika na wachezaji nguli duniani ambao walijumuisha pia viongozi wa FIFA imekuwa na hamasa ya aina yake huku Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Mohamed Mchengerwa akifungia timu yake goli moja.
Mechi hiyo imechezwa mara baada ya kumalizika mkutano mkuu wa 44 wa CAF uliofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha huku ukihudhuriwa na zaidi ya washiriki mia tano kutoka nchi 58 duniani ambapo nchi wanachama ni 52 ukiondoa Kenya na Zimbabwe ambazo hazikushirriki kutokana kuwa zilikuwa zikitumikia adhabu.
Awali, Dkt Abbasi akihojiwa na waandishi wa habari amefafanua kuwa mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa ya kimichezo na kiuchumi kwa nchi yetu.
"Ni muhimu kutambua kuwa Serikali imetumia mkutano huu mkubwa wa michezo kimkakati ili kuitangaza Tanzania" ameongeza
Aidha, Dkt Abbasi amesema kupitia mkutano huo Rais wa FIFA ametangaza kuziongeza timu za Afrika katika mashindano ya FIFA, pia kuongeza ufadhili kwa nchi za Afrika.
Kuhusu kuandaa AFCON mwaka 2027 Dkt. Abbasi amesema Tanzania imeshauriwa kushirikiana na Uganda kuandaa mashindano hayo.
Tags:
HABARI