Kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alilolitoa April 8 mwaka huu la kuwataka viongozi kutoa elimu na mafunzo kwa Watanzania ili wajitokeze kushiriki Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimewakumbusha Wahitimu wote wa Digrii za uzamivu, umahiri, stashahada za uzamili na digrii za awali kujiandaa kuhesabiwa.
Rai hiyo imetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof William Anangisye wakati akizungumza na Wahitimu wa duru ya kwanza katika Mahafali ya hamsini na mbili yaliyofanyika leo Juni 2 Katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam.
Anangisye amebainisha kuwa ushiriki wa Wahitimu hao utasaidia Serikali kupata Takwimu za msingi zitakazo ainisha mahitaji halisi ya wananchi na hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji wa mazingira yaliyopo.
Katika hatua nyingine Anangisye amesema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimepiga hatua katika miradi mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu .
Ameitaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka UDASA mpaka zilizopo ofisi za Kurugenzi ya Miliki, ukarabati wa mabweni ya wanafunzi na kukamilika kwa ujenzi wa Tenki la Maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita laki tano (500,000) za maji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la chuo Kikuu cha Dar es Salaam Jaji Mstaafu Damian Lubuva amewataka Wahitimu kufanya bidii kutafuta fursa za kuendeleza maisha pamoja na kua na ushirikiano na umoja katika kila wanalolifanya.
Amesema baraza linawasisitizia wanataaluma kufanya bidii katika kufanya tafiti kwenye maeneo yatakayogusa maisha ya watanzania ili tafiti hizo zigoe majibu ya matatizo yaliyoko kwenye jamii.
Ameongeza kuwa baraza liko macho kuhakikisha kuwa sera na miongozo mbalimbali inayopitishwa inafanyiwa kazi kwa kuzingatia malengo makuu ya Chuo.
Akizungumza kabla ya kutunuku Digrii za Uzamivu, Umahiri, Stashahada za Uzamili na Digrii za awali Mkuu wa Chuo hicho Rais Msataafu wa Awamu ya 4 Jakaya Mrisho Kikwete akawakumbusha Watanzania kujitokeza kuchanja chanjo ya Uviko-19 kwakua Corona bado ipo.