MADADA POA, KELELE ZA MUZIKI KILIO WILAYA YA KINONDONI, DC GODWE ATOA MAELEKEZO


PICHA ZOTE NA YUSUPH DIGOSSI 

Na Yusuph Digossi- Sauti za Mtaa Blog 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe  amewataka wamiliki wa Baa na Kumbi za starehe kuendesha shughuli zao bila kufanya uchafuzi wa kelele kwa wananchi wanaokaa karibu na shughuli hizo.

Gondwe alitoa maelekezo hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Wananchi wa mtaa wa chuo Kikuu Nzasa ambao wamelalamikia changamoto ya makelele nyakati za usiku  na uwepo wa idadi kubwa ya madada poa kutoka katika bar na kumbi za starehe zilizopo karibu na  Mtaa huo .


Wakizungumza katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ambapo waliwasilisha malalamiko yao baadhi ya wakazi wa eneo hilo la mtaa wa Nzasa Chuo Kikuu , wamesema wamekuwa wakikumbana na adha kubwa ya kelele nyakati za usiku ambayo inazalishwa na muziki.


Mwenyekiti wa mtaa huo Dr Edwinus C Lyaya  amesema Bar hizo zimekuwa zikikiuka sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ambayo imeelekeza sauti ya muziki kwa nyakati za usiku isizidi 'Decibel 40' lakini Bar hizo zimekuwa zikizidisha kiwango cha Sauti na kupelekea kero kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.


Lyaya amesema kuwa changamoto nyingine ni ongezeko la madada poa ambao wamekuwa wakifanya biashara hadi nyakati za asubuhi jambo ambalo ni tishio kwa maadili na afya za watoto katika maeneo hayo.


Naye Mjumbe wa Nyumba 50 wa mtaa huo Mariam Sepetu amesema kuwa wakazi wa mtaa huo hawamkatazi mtu kufanya Biashara isipokuwa anatakiwa kufata sheria na taratibu kwa mujibu wa kibali alichopewa na serikali


Akizungumza baada baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa mtaa huo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe amekiri kuwepo kwa tatizo la upigwaji wa muziki bila kufata sheria na taratibu zilizopo huku akiahidi kuanzisha operesheni maalumu itakayoambata na utolewaji wa elimu kwa Wanachi na wamiliki wa bar ili kuondokana na adha hiyo.


" Niwape pole sana wakazi wa Nzasa , nalifahamu suala hili na tumeendelea kulifanyia kazi suala hili ili kuhakikisha kelele Wilaya ya Kinondoni zinapungua.

Kuhusu changamoto ya uwepo wa Madada poa katika Wilaya hiyo Gondwe ametoa rai kwa wazazi na walezi kutoa malezi bora kwa watoto ili kutengeneza kizazi bora siku za usoni.


Katika hatua nyingine Gondwe alitoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kinondoni kuwa na Utamaduni wa kushiriki mikutano ya mtaa ili kuwasilisha changamoto zinazowakabili ili kuepusha migongano isiyokuwa ya lazima.


Post a Comment

Previous Post Next Post