KAMISAA MAKINDA AWAONYA WENYE TABIA YA KUCHUKUA RUSHWA KWENYE ZOEZI LA SENSA 2022.


Na Hadija Bagasha Tanga, 

Kamisaa wa sensa,  Anna makinda amewaonya maofisa wa serikali wenye tabia ya kuwaomba pesa wafanyakazi wao ambao wanaoomba ruhusa kwajili ya kwenda kushiriki kwenye nafasi za ukarani  kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi kuacha tabia hiyo mara moja kwani jambo hilo ni kinyume cha sheria.  

Kamisaa amesema hadi hivi zoezi la mchakato wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 umefikia asilimia 81.

Kamisaa amesema zoezi hilo kwa mwaka huu katika nafasi za ukarani zitatumiwa kuombwa kwa njia ya mtandao tofauti na miaka mingine ili kuepusha kulifanya kwa kujuana na kwa upendeleo. 


Kamisaa ametoa kauli hiyo kwenye kikao cha 17 cha maafisa habari wa serikali na taasisi za umma jijini Tanga ambapo ametumia nafasi hiyo kupiga marufuku baadhi ya waajiri ambao wana tabia ya kuwaomba fedha watu pindi wanapoomba ruhusa ya kutaka kwenda kuomba ukarani wa sensa. 

"Nasikia hasa wale waajiri mwajiriwa atakayetaka kuomba lazima aombe ruhusa kwa mwajiri wake tunaambiwa baadhi ya waajiri wanawadai hao makarani fedha nasema hiyo ni marufuku na ni kosa kabisa na wewe mwenyewe unayeomba kwani hujiamini mpaka uanze kumtolea mtu fedha? Alihoji Kamisaa Makinda. 


Kamisaa alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa watendaji wa kata na vijiji kuacha kuwatoza fedha pindi watu wanapohitaji kugongewa mihuri na kufafanua kuwa sensa ni ya watu wote kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla. 

Aliwataka makarani wanaoomba kushiriki zoezi hilo wajiamini na kusema kuwa asitokee mtu yeyote kuchukua pesa kwasababu ya makarani jambo ambalo sio sahihi na kuwaasa watendaji kutochukua pesa kwa mtu yeyote anayeomba ukarani. 

Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya ardhi Dkt. Allan Kijazi amesema kuwa hapa anasisitiza umuhimi wa sensa ya watu na makazi huku akisema zoezi hilo linakwenda kuisaidia nchi kuandaa mikakati na mipango itakayoweza kuboresha makazi ya wananchi kulingana na idadi ya watu waliopo. 



"Katika mikakati ya serikali mojawapo ya mikakati ya kitaifa na pia kwenye mikataba ya kimataifa ambayo tumeingia hasa katika masuala ya makazi ni kwamba serikali inayo wajibu wa kuandaa mikakati na mipango ambayo itaboresha makazi ya wananchi wake hivyo lazima tupate taarifa sahihi za hali ya makazi ilivyo katika vijijo vyetu na katika miji yetu, "alisistiza Dkt. Kijazi. 

Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya habari,  mawasiliano na teknolojia ya habari Dkt. Jimmy Yonazi amesema kila mwananchi atafikiwa katika zoezi hilo na lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anashiriki katika uchumi kwa maana ya kwamba anajulikana yuko wapi ili aweze kupokea huduma za serikali lakini vilevile ashiriki katika kuchangia uchumi wake na hatimaye kufanya shughuli za kimaendeleo. 



"Jambo hili litamuwezesha hata mwananchi kushiriki katika uchumi wa dunia kwamaana ya kwamba kama anaagiza bidhaa aweze kuagiza bidhaa zake kutoka mahali popote duniani na ziweze kumfikia, "alisema Yonazi. 

Katika zoezi hilo kamisaa huyo amefafanua kuwa watendaji wa vijiji na kata hawataruhusiwa kuomba nafasi hiyo kwa kuwa wao watakuwa sehemu ya usimamizi wa mchakato. 





Post a Comment

Previous Post Next Post