Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya mradi wa ushirikiano wa wasindikaji na wazalishaji katika tasnia ya maziwa Tanzania kati ya Benki ya kilimo Tanzania na Taasisi ya BILL and MELINDA GATES, Machi 07, 2022 jijini Dar es Salaam |
Na Mwandishi wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) uhakikishe fedha ya mikopo kwa wakulima wadogo zinatumika ipasavyo na kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Benki ya Maendeleo ya Kilimo izingatie agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kwamba fedha kwa ajili ya mikopo zinatumika ipasavyo, zinawafikia wakulima wengi zaidi wakiwemo wakulima wadogo na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumatatu, Machi 7, 2022) wakati wa uzinduzi wa mradi wa ushirikiano wa wasindikaji na wazalishaji katika tasnia ya maziwa kwenyw ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.
Mradi huo unalenga kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya maziwa kupitia uhamasishaji wa uwekezaji kutoka sekta ya umma na sekta binafsi kwa kusudi la kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, kuongeza ukusanyaji wa maziwa katika mfumo ulio rasmi, kukuza uwezo wa viwanda katika uchakataji wa maziwa, na kupanua wigo wa soko la bidhaa za maziwa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi iimarishe eneo la utafiti hasa kwenye vyuo vya utafiti kwa kufanya tafiti ambazo zitatoa suluhisho kwa changamoto katika sekta ya mifugo ili kuongeza ubora na wingi maziwa.
Waziri Mkuu alishuhudia uwekaji saini wa makubaliano yakayowezesha ufanikishaji wa mradi huo baina ya Benki ya Kilimo (TADB) na taasisi ya Bill & Melinda Gates wenye thamani ya dola za Marekani milioni saba.
Mapema, akielezea mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege alisema mradi huo wa miaka mitatu unalenga kuwafikia wafugaji 100,000 na viwanda kati ya 9 hadi 12 ambavyo vitasaidiwa kuandaa mikakati thabiti ya kibiashara na masoko ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa maziwa.