Na Yussuph Digossi- Sauti za Mtaa
Mchezo wa ligi kuu ya NBC kati wenyeji Simba dhidi ya Dodoma umemalizika katika uwanja wa Benjamini Mkapa, mwenyeji anaondoka na alama tatu muhimu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 .
Mabao ya Clotus Chama aliyefunga kwa Mkwaju wa penati mnano dakika ya 57 na Meddie Kagere dakika ya 75 yalitosha kupeleka kilio kwa walima zabibu wa Dodoma Jiji .
Kipindi cha kwanza Dodoma walionekana kuwa wagumu , Simba walianza mchezo kwa kasi na kupiga pasi fupifupi kuelekea lango la wapinzani wao na kutengeneza nafasi kadhaa lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Dodoma Jiji ikiongozwa na beki kisiki George Amani Wawa iliwanyima nafasi ya kuandika bao la kuongoza
Dodoma walionekana kuingia na mbinu kucheza kwenye eneo lao la ulinzi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kupitia mshambuliaji Seif Karihe ambae alishindwa kutamba mbele ya walinzi wa Simba .
Nahodha John Rafael Bocco alishindwa kuendelea na mchezo mnamo dakika ya 28 na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere .
Kipindi cha pili Simba walirejea kwa kasi na iliwachukua dakika 12 tu kuandika bao la kwanza kupitia kiungo Clotus Chama kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi George Wawa kuunawa mpira katika eneo la hatari na dakika 75 Meddie Kagere akaandika bao la Pili.
Baada ya ushindi huo Simba inafikisha alama 37 baada ya kushuka dimbani mara 17 ikiwa ni tofauti ya alama 8 na wapinzani wao Yanga Sc ambao ni vinara wa ligi.
Nyuso za mashabiki wa Simba zilionekana kuwa na furaha baada ya kuwaona wachezaji wao Thadeo Lwanga na Kibu Denis wakirejea uwanjani baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi .