Airtel Tanzania yazindua maduka manne ya Kisasa Jijini Dar es Salaam.




Kampuni ya Airtel Tanzania imezindua maduka manne mapya ya kisasa katika maeneo ya Kawe, Sinza, Mikocheni na Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni juhudi za kuwapunguzia wananchi gharama na usumbufu wa kusafiri kufuata huduma za kampuni hiyo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Airtel, Adriana Lyamba, amesema uzinduzi huo umeongeza idadi ya maduka ya Airtel jijini Dar es Salaam kufikia kumi, huku yote yakitoa huduma bora na za kisasa kwa wateja.

“Leo tumezindua tena maduka manne Jijini Dar es Salaam, na kufanya jumla ya maduka kuwa kumi. Hii itawawezesha wananchi kupata huduma karibu na walipo bila kuhangaika,” alisema Lyamba, akihimiza wananchi kuyatumia maduka hayo kikamilifu kwa ajili ya huduma bora.

Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Maduka ya Airtel, Gaspa Ngowi, alisema maduka hayo yataweza kutoa huduma zote zinazopatikana katika makao makuu ya Airtel. Huduma hizo ni pamoja na usajili na ubadilishaji wa laini za simu, huduma za Airtel Money kwa wateja na mawakala, mauzo ya simu janja, vifaa vya Home Broadband kama router za 5G na MiFi, pamoja na kurejesha akaunti au kubadilisha nywila za Airtel Money.

Ngowi aliongeza kuwa wananchi wa maeneo husika wanapaswa kutumia fursa hiyo kupata huduma karibu na makazi yao ili kupunguza gharama na muda wa kufuata huduma mbali.

Airtel imesisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya ahadi yake ya kuwahudumia wateja wake kwa viwango vya juu na teknolojia ya kisasa kote nchini Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post