Na. Veronica Mwafisi-Arusha
Mameneja
Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMnet) wamemuunga mkono Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza
sekta ya utalii katika nchi zao baada ya kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro
ambayo ni moja ya vivutio maarufu duniani.
Akiongoza
ziara ya Mameneja hao baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano Mkuu wa 9 wa Rasilimaliwatu
katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMnet), Rais wa Mtandao huo ambaye pia ni
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema waliona ni vema Mameneja hao kutoka nchi mbalimbali wakatembelea
Hifadhi hiyo ili kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ambaye amekuwa mstari wa mbele kutangaza sekta ya utalii ili kukuza uchumi wa
Tanzania.
“Tuliona si jambo jema
viongozi hawa wa Rasilimaliwatu wakarudi nchini kwao bila kufanya utalii, hivyo
tukaamua kuratibu safari ya kwenda Ngorongoro kwani kwa kufanya hivyo tunaamini
watatusaidia kwenda kutangaza utalii wa Tanzani katika nchini zao na kukuza
pato la taifa.” Bw. Daudi amesisitiza.
Bw. Daudi amesema Mameneja hao wameweza kuona
vivutio mbalimbali katika Hifadhi hiyo ya Ngorongoro ikiwemo wanyama, mandhari ya
kuvutia pamoja na kujifunza masuala mbalimbali.
Mkutano wa 9 wa Mtandao wa Mameneja
Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) uliofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umehitimishwa rasmi baada ya kufanyika
kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 4 hadi 7 Novemba, 2024 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha.
Mkutano huo ulibebwa na Kaulimbiu isemayo ‘Utawala Stahimilivu na Ubunifu: Kukuza Sekta ya Umma
ijayo kupitia Uongozi wa Rasilimaliwatu’.