Kikundi cha COCOBA kijulikanacho kama TUSHIKANE, katika kijijini cha Mkata Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro, kinamatarajio makubwa ya mauzo ya vitunguu na kupata zaidi ya Bilioni moja, kupitia mradi wao wa kilimo cha vitunguu baada ya kupata fedha za Mradi kutoka Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Akieleza juu ya maendeleo ya kikundi chao, Mwenyekiti wa kikundi cha TUSHIKANE Bw. Daniel Gaspar, amesema REGROW imewapatia zaidi ya Milioni 12 ambazo wamezitumia kulima vitunguu na kukopeshana kwa ajili ya biasha binafsi.
Bw. Gaspar ameongeza kuwa baada ya kupata elimu ya matumizi sahihi ya fedha na kilimo, Mwaka 2023 walianza kilimo cha vitunguu na sasa wanatarajia kulima heka zaidi ya tano huku heka moja ikiwa inakadiriwa kukipatia kikundi hicho Shilingi Milioni 200 na kwa heka tano kupata Shilingi Bilioni moja baada ya mauzo.
Aidha Bw. Gaspar ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwajali na kuwapelekea mradi wa REGROW ambao umebadili maisha yao kutoka kwenye umasikini na kuwa na vipato vya uhakika.
Kaimu Msimamizi wa Mradi wa REGROW Bi. Blanka Tengia, amesema kuwa mradi huo wa kimkakati, unaoendeshwa na fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na kutekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, unaendelea kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania kwa maslai mapana ya Taifa kwa ujumla.