Na Yusuph Digossi
WAKILI wa kujitegemea James Marenga amesema kuwa sheria ya habari inayohusu kashfa na jinai kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.
Marenga ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wahariri wa magazeti ya mwananchi.
Amesema, kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ndani ya sheria hizo kuna maeneo mwandishi anaweza kujikuta anaingizwa mkenge hata kwa nia njema ya habari aliyoiandika kwa taifa lake. Ndio maana tumeona kuna kila sababu ya kufanyia maboresho,” amesema Wakili Marenga.
Hata hivyo Wakili Marenga ameongeza kuwa sheria ya habari inayohusu kashfa kuwa jinai, inakulinda pale tu kauli hiyo inayoweza kutafsiriwa kuwa ya kashfa, imetolewa bungeni ama na rais, basi.
“Pamoja na kwamba mwandishi amelindwa katika kipengele hicho, lakini bado sheria hiyo hiyo haimpi kinga kama habari hiyo itakwaza viongozi wa juu. Unaweza kuandika ila inategemea itapokelewa vipi.
“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo.
“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasehma sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,” amesema Wakili Marenga.
Wakili Marenga amekutana na Lilian Timbuka, mhariri wa habari Mwananchi pia Samuel Kamdaya, Mahariri wa Habari wa The Citizen kuzungumzia mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari nchini.
Tags:
HABARI