Makambusho ya Taifa nchini imesema imejipanga kutumia njia mbalimbali za kuongeza idadi ya Watalii wa ndani na nje ya nchi kwa lengo kuongeza Mapato ya taasisi hiyo pamoja na kuendelea kudumisha tamaduni za Kitanzania kwa Ustawi bora wa Taifa.
Ameyasema hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Luoga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu onesho maalumu la Sanaa Pamoja Utalii Endelevu lililoandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya Nafasi Art Space litakalofanyika Mei 27 mwaka huu Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es salaam.
"Programu ya Museum Art Explosion inaendana na Lengo la serikali ya kuhamasisha utalii wa utamaduni hivyo kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kazi kubwa ya Royal Tour" alisema Luoga
Aliongeza kuwa Kazi ya Royal Tour ni kufungua fursa mbalimbali za utalii nchini Tanzania na wao kama makumbusho ya Taifa wanaichukulia kama fursa ya kutangaza utalii wa asili na utamaduni.
Pia Luoga alisema katika mpango mkakati wa miaka mitano wa Taasisi yao 2021/22-2025/26 wanampango wa kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi na kuongeza mapato ya Taasisi.
Kwa upande wake Mratibu wa Sanaa za Jukwaani kutoka Nafasi Art Space Kwame Mchauru alisema katika tukio hilo kutatanguliwa na Mdahalo kuhusu kazi ya Sanaa kabla ya uzinduzi wa Kampeni ya Sanaa Pamoja ambayo itakuwa ikiendelea mwaka mzima kwa lengo la kuchangia ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Wananchi wa Mataifa ya Afrika.
Kupitia mradi huo wa Sanaa pamoja pia wanaangalia njia yambalimbali za kiubunifu zenye kukutanisha taaluma mbalimbali za kisanii pamoja ili kuunda Jumuiya ya Wabunifu inayosukuma maendeleo ya kazi mpya.
Tags:
HABARI