Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ametoa wito kwa wadau wa elimu kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kutoa maoni yatakayowezesha uboreshaji wa Sera hiyo ambao unakwenda sambamba na uboreshaji wa mitaala.
Waziri Mkenda amesema hayo leo Machi 30, 2022 Jijini Dodoma alipokutana na Viongozi wa Dini na Wamiliki wa Shule Binafsi kwa ajili ya kupokea maoni ya maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala hiyo.
"Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inahitaji kufanyiwa mapitio ili iweze kuendana na mazingira ya sasa na iweze kutekelezeka," amesema Prof. Mkenda.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo amewashukuru Viongozi wa Dini na Wamiliki wa Shule binafsi kwa kushiriki katika mkutano huo muhimu wa kutoa maoni ambayo yatasaidia kuboresha Sera na Mitaala ili watoto wa Kitanzania wapate elimu itakayowapatia ujuzi na kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa dini na wamiliki wa shule wamesema elimu ni msingi wa kila kitu hivyo pamoja na mambo mengine umakini kwenye lugha ya kufundishia unahitajika kwa kuhakikisha lugha ya Kiswahili na Kingereza zinatumika.
Tags:
HABARI