Na. Projestus Binamungu
WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kukamilika kwa vituo viwili vya michezo vinavyojengwa katika mkoa wa Tanga na Dar es Salaam ni mwanzo mzuri wa kuzalisha timu bora ya taifa ya mchezo wa soka.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Machi 12, 2022, wakati alipotembelea mradi wa kituo cha Michezo kinachojengwa katika eneo la Kisarawe Two , Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutembelea majengo mbalimbali yanayojengwa kama sehemu ya mradi huo Waziri Mchengerwa amesema, kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho na kile kinachojengwa mkoani Tanga utasaidia kutoa hifadhi ya mafunzo katika mpango kabambe wa kuendeleza vipaji vya michezo nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa ambao unatarajiwa kuanza kutekelezwa kupitia wizara yake.
“Ni lazima tukiri kwamba anguko la mchezo wa soka hapa nchini linachangiwa kwa kiwango kikubwa na miundombinu hafifu ya michezo, kwa hiyo uwepo wa viwanja hivi vyenye sifa za kimataifa utasaidia kukuza vipaji vya michezo hasa katika mpango wetu wa Wizara wa kuibua vipaji nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa”. amefafanua Waziri Mchengerwa.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) Wallace Karia, amesema ujenzi wa kituo hicho cha michezo cha Kigamboni unagharimu dola bilioni mbili na elfu 78 ambapo mradi huo unatarajiwa kuwa umekamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Awali Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusuph Singo amesema pamoja na ujenzi wa vituo hivyo viwili vya michezo, Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo tayari ipo kwenye hatua za mwisho kabisa za kuvifanyia ukarabati mkubwa viwanja vya michezo katika shule teule 56 pamoja na kuboresha miundombinu katika kituo cha michezo cha maendeleo ya michezo cha Malya.