Na Yussuph Digossi- Sauti za Mtaa Blog
Matumaini ya kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi kuu ya Uingereza yanazidi kuwa finyu kwa mashabiki wa Manchester United.
Hali hiyo inakuja baada ya kikosi cha Manchester United kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa mahasimu wao Manchester City katika uwanja wa Etihad.
Ni kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji Kevin DeBruyne alianza kupeleka maumivu kwa Manchester United mnamo dakika 5 baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na mpishi Bernado Silva .
Wachezaji wa Manchester City wakishangilia bao katika mchezo wa Ligi kuu ya Uingereza dhidi ya Manchester United ( picha na mtandao wa Manchester City) |
Kiungo mshambuliaji Jadon Sancho akaisawazishia Man U dakika ya 22 akiunganisha pasi safi ya kiungo Paul Pogba, lakini hiyo haikuwa sababu ya kuifanya Man City kuendeleza mauaji kwa mahasimu wao baada ya Kevin Debruyne kupachika bao la 2 dakika ya 28, na kuifanya Manchester City kwenda vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha Pili Manchester City walianzia pale walipoishia Dakika ya 68 Riyad Mehrez akapachika bao la tatu na la nne dakika ya 93 kukamilisha ushindi mnono kwa kikosi cha Manchester City na kuendelea kujikita kileleni baada ya kukusanya alama 69.
Baada ya kichapo cha leo Manchester United wanaendelea kusalia nafasi ya 5 wakiwa na alama 47