Mkurugenzi wa Leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Andrew Mkapa, akisoma hotuba ya ufunguzi wa warsha juu ya Uwasilishaji wa Kanuni za Wamiliki Wanufaika, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, katika ukumbi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro leo tarehe 31 Machi, 2022 jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Meinrad Rweyemamu, akiwasilisha mada juu ya Wamiliki Wanufaika kwa washiriki wa warsha iliyofanyika katika Ukumbi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, jijini Arusha tarehe 31 Machi, 2022.
Washiriki wa warsha ya uhamasishaji kuhusu Uwasilishaji wa Kanuni za Wamiliki Wanufaika, wakisilikiza mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wawezeshaji kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika ukumbi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, jijini Arusha leo tarehe 31 Machi, 2022.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano BRELA
31 Machi, 2021- Arusha
Wamiliki wa Kampuni ambao hawajatekeleza hitaji la kisheria la kuwasilisha taarifa za Wamiliki Wanufaika wametakiwa kutumia muda uliobaki kukamilisha zoezi hili, ili kuepuka
adhabu zisizo za lazima.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa ambaye amewakilishwa na Mkurugenzi wa Leseni Bw. Andrew Mkapa, katika ufunguzi wa warsha ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za Wamiliki Wanufaika iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, jijini Arusha tarehe 31 Machi, 2021.
Bw. Nyaisa ameeleza kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Muswada wa Sheria ya Fedha, 2020, lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Makampuni, Sura ya 212 kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za Wamiliki Wanufaika (Beneficial Owners), katika kampuni ambazo taarifa zao ni muhimu kwa sababu za kikodi pamoja na kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, rushwa na ufadhili wa vitendo vya
ugaidi.
"Kanuni zilianza kutumika mwezi Mei, 2021 ambapo kutokana na muda uliokuwa
umesalia kuwa mfupi kwa kampuni zilizokuwa zimesajiliwa kabla ya tarehe 1 Julai, 2020, Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Makampuni aliongeza muda wa uwasilishaji taarifa kwa kipindi cha mwaka mmoja ambacho kilisha
tarehe 31 Disemba, 2021 na baada ya hapo kiliongezwa hadi tarehe 1 Julai, 2022",
amesisitiza Bw. Nyaisa.
Naye Bw. Praygod Manase Wakili kutoka kampuni ya Uwakili ya Mawala amesema,
kanuni hizi zitasaidia kuwafahamu wamiliki halali wa makampuni na kuondoa utendaji
kazi bila kufuata mifumo wa kiserikali.
Kupitia kanuni hizi zitasaidia kuwaondoa
wanaoonekana ni wamiliki wa kampuni na kupata faida wakati hawahusiki na wale
wahusika halali wanapoteza haki zao.
"Hapo awali bila kanuni hizi kulikuwa na athari kubwa kwasababu ilikuwa ni kawaida kwa mtanzania ambae kiuhalisia siyo mmiliki wa kampuni kutangulizwa mbele na kutambulika kama mmiliki wa kampuni hiyo, wakati nyuma ya hiyo kampuni wamiliki halali siyo watanzania, hivyo vitendo hivi vilikuwa vinaipotosha Serikali", amesema Bw. Manase.
Bi. Aishinile Maimu, Wakili kutoka Kampuni ya Uwakili ya Kisaka and Consult
amehitimisha kwa kuishukuru BRELA kwa kuandaa warsha hiyo hasa kwa kuwakaribisha Mawakili kwasababu itasaidia katika utekelezaji wa kanuni hiyo hasa wanapotoa msaada wa kisheria kwa wadau wenye umiliki wa kampuni ndani na nje ya nchi
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano-BRELA
Tags:
BIASHARA