Watanzania wamesisitizwa kuwa na matumizi Bora na fanisi ya Nishati kwa kupunguza matumizi makubwa ya Nishati yasiyoyalazima ikiwemo upotevu wa umeme ambao utapunguza gharama na kulinda mazingira.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga wakati akitoa taarifa ya Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati unaotarajiwa kufanyika Desemba 4 hadi 5 mwaka huu Jijini Arusha ambapo Mgeni Rasmi ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko.
“Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP, Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Ireland na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wameandaa mkutano wa kikanda wa matumizi bora ya Nishati utakaofanyika Desemba 4 hadi 5 jijini Arusha mkutano huu utasaidia kuendelea kutoa uelewa kwa watanzania kuhusu umuhimu wa Matumizi Bora ya Nishati “ Amesema Mhandisi Luoga.
Aidha amesema kuwa mkutano huo utahusisha wadau wa nishati takribani 400 wa ngazi mbalimbali ikiwemo Mawaziri, wataalam na sekta binafsi, ambapo watabadilishana uzoefu na uelewa katika masuala ya nishati, fursa zilizopo na uwekezaji.
Hata hivyo, amesema utekelezaji wa mradi huo,Tanzania tayari imeshaandaa mkakati wa matumizi bora ya nishati kwa miaka 10 (2024-2034), huku wakitoka ufadhili kwa wanafunzi wa kike katika masula ya nishati ambao wana ujuzi mkubwa wa kushauri namna bora ya utumiaji nishati bora kwa gharama ndogo zaidi.
Kuhusu programu ya matumizi bora ya Nishati, Mhandisi Luoga amesema ina umuhimu mkubwa nchini kwani inahusisha matumizi ya umeme kwa ufanisi na kwa ubora, inalenga kupunguza upotevu wa umeme, kupunguza gharama za umeme na kulinda mazingira.
“Uelewa zaidi bado unahitajika kwa watanzania kuhusu matumizi bora ya Nishati hususani Majumbani ambapo wanaweza kununua vifaa ambavyo havitumii kiasi kikubwa cha umeme mfano taa, friji na majiko ya kupikia Ili kuokoa unit za umeme ambao utapunguza gharama na kuwa msaada kwa wengine” Ameongeza Mhandisi Luoga.
Kwa upande wake, Mtaalam wa Miradi kutoka UNDP, Abbas Kitogo, amesema Mkutano huo wa kikanda, utakuwa ni sehemu kutoa uelewa kuhusu faida ya matumizi bora ya Nishati kwa watanzania na makampuni mbalimbali pamoja na kubadilisha ujuzi, uelewa Ili kuwa na mtazamo mmoja katika matumizi bora ya nishati.
Naye, Naibu Balozi wa Ireland nchini, Mags Gaynor amesema Ubalozi huo unafurahishwa na jinsi Tanzania inavyotekeleza Programu ya Matumizi Bora ya Nishati ikiwemo kuandaa mkakati utakaopelekea Tanzania kutekeleza kwa ufanisi zaidi programu hiyo.
Hata hivyo amesema mkutano huo ni hatua kubwa katika safari ya mabadiliko kuelekea kwenye matumizi bora ya nishati pamoja na kuwa njia ya kusukuma ajenda ya matumizi bora ya nishati.
Programu Meneja wa Miradi ya Nishati kutoka EU, Massimiliano Pedretti, amesema Umoja huo utaongeza muda wa utekelezaji wa programu ya Matumizi Bora ya Nishati nchini ambayo ilikuwa ifikie ukomo mwaka 2024 lakini itaisha mwaka 2025 pamoja na kutanua wigo wa kazi na ufadhili hii ni kutokana na Jitihada za serikali za kuwezesha matumizi bora ya Nishati.