CDF YAZINDUA MRADI WA KUHAMASISHA JAMII KUZUIA UKATILI WA KINGONO KWA WATOTO




Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) limezindua  rasmi Mradi mpya wa uhamasishaji jamii kuzui ukatili wa kingono kwa watoto utakaotekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma ambao utatekelezwa kwa miaka miwili (2) katika kata mbili za Wilaya ya Mpwapwa ambazo ni Pwaga na Lupeta.

 
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Febuari 28, 2024 katika Ukumbi wa ofisi za CDF Mpwapwa Mkurugenzi wa shirika hilo amesema kuwa Lengo kuu la Mradi huo ni kupunguza kuenea kwa vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto hasa watoto wa kike kwa kuhamasisha jamii kuzuia ukatili huo. 



Amesema "Kupitia Mradi, shirika la CDF litafanya kazi na watoto walioko ndani ya shule, waalimu na menejimenti ya shule, viongozi wa serikali, wamiliki wa nyumba za kupanga, wahudumu wa afya, wazazi pamoja na vikundi vya kina baba ambavyo CDF inafanya navyo kazi katika kata hizi mbili". 


Ameongeza kuwa Ili kufikia malengo ya Mradi huu, CDF itafanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuwajengea uwezo watoto kwa kuwapa elimu ya afya ya uzazi na namna ya kuzuia ukatili wa kingono, kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waweze kutoa huduma bora na rafiki za afya ya uzazi kwa vijana balehe na shughuli nyinginezo. 





"CDF itashirikiana na watumishi mbalimbali wa Serikali katika halmashauri ya Mpwapwa waliopo katika ofisi ya Ustawi wa Jamii, idara ya Maendeleo ya Jamii, idara ya elimu, ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Dawati la polisi la jinsia na watoto, Mahakama ya Wilaya, watendaji Kata na Vijiji kutoka kata za Lupeta na Pwaga pamoja na wadau wote wa ulinzi wa mtoto waliopo katika Wilaya ya Mpwapwa". amesema 




Aidha Mkurugenzi mtendaji huyo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri unaoliwezesha shirika hilo kuendelea kufanya shughuli zake. 

Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) ni shirika la hiari lisilo la kiserikali, lililosajiliwa mwaka 2006 chini ya sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali namba 24/2002 ambapo lLengo kuu la shirika hilo ni kutekeleza programu na mipango mbalimbali yenye kukuza, kutetea na kuboresha haki na ustawi wa mtoto wa Kitanzania.


Post a Comment

Previous Post Next Post