Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewataka Wakala wa uchimbaji wa Visima na ujenzi wa mabwawa DDCA, kufufua visima zaidi ya 197 ambavyo vilianza kuchimbwa ili vianze kuingiza maji kwenye mfumo na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Waziri Aweso ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 03, 2022 alipokua akikagua mitambo ya kisasa ya kuchimba visima ambayo imenunuliwa na serikali hivi karibuni na kuzungumza watumishi wa kitengo hicho Jijini Dar es salaam ambapo aliwataka wakala hao kuanza kazi hiyo mara moja ili wakazi wa Dar es salaam na Pwani waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.
Pia Waziri Aweso amewataka watanzania kusimamia na kutunza vyanzo vya maji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira ili kuweza kuepuka uchafuzi wa maji pamoja na vyanzo vyake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijini RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amemshukuru Waziri Aweso kwa kusimamia sekta ya uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa na kuwawezesha kufanya kazi kwa nguvu na ufanisi.
Naye Mkuu wa wilaya ya Ubungo Heri James amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya maji kwa namna anavyokabiliana na changamoto ya uhaba wa maji kwa kuchukua hatua za haraka kuondoa adha hiyo kwa wananchi ili waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.
Tags:
HABARI