Na John Mapepele, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo Agosti 10, 2022 amefungua Mkutano Mkuu wa 44 wa kawaida wa CAF katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) Arusha.
Akifungua mkutano huo Mhe.Majaliwa amefafanua mafanikio mbalimbali ya michezo ambayo yamepatikana katika kifundi kifupi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ametoa wito kwa wageni waliohudhuria mkutano huo kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii na kujionea vivutio vya utalii.
Mkutano huo umehudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Patrick Motsepe ambapo Mhe. Majaliwa aliwapatia zawadi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kwa sasa Tanzania imepiga hatua mkubwa katika michezo kiasi cha kuweza kuratibu mikutano mikubwa ya kimataifa kama huu.
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino amesisitiza kuwa kipaumbele cha FIFA kwa sasa ni kuimarisha timu za taifa ili ziweze kufanya vizuri ambapo ameongeza kuwa katika kipindi hiki Afrika imeongezewa timu ambazo zitashiriki kombe la dunia.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Said Yakubu.
Zaidi ya Waandishi wa Habari mia moja wa ndani na nje ya Tanzania wamealikwa ambapo inatarajiwa watu zaidi ya bilioni moja kutazama mbashara mkutano huu.
Tags:
MICHEZO