REA YATUMIA TAKRIBANI TRILIONI 3 KUFIKISHA UMEME VIJIJINI, YAWEKA REKODI KWA NCHI ZA KUSINI MWA JANGWA LA SAHARA




Wakala wa Nishati Vijijini (REA) hadi sasa umetumia takribani Shilingi trilioni 3 kwa ajili ya kazi ya kupeleka miradi ya umeme vijijini ili kuhakikisha nishati ya umeme inafika na kutumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji, kuboresha huduma na shughuli za kiuchumi.

Hayo yamesemwa Agosti 11, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy wakati wa mkutano wa Wakala huo na wadau wake kuelezea masuala mbalimbali ya nishati vijijini uliorushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam ambapo amesisitiza kuwa mradi unaoendelea hivi sasa (mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili) pekee unagharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.2.


Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, kutokana na kazi zinazoendelea na mipango waliyoijiwekea, vijiji vyote nchini vitapata umeme kabla ya muda ulioelekezwa (mwaka 2025).

"Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeahidi kufikisha umeme katika vijiji vyote ifikapo mwaka 2025, sisi kama REA hatutafika huko, tutakamilisha vijiji vyote kuvipatia umeme kabla ya mwaka huo" alisema Mhandisi Saidy na kuongeza kuwa

"Wananchi wakipata nishati ya umeme itasaidia sana katika uhifadhi wa mazingira, kwani hivi sasa zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa jambo ambalo linapelekea kuathiri mazingira kwa kuharibu misitu. Takwimu zinaeleza kuwa kwa mwaka mmoja, Tanzania inapoteza hekta 400 za misitu"

Ameendelea kwa kusema kuwa, REA inatumia gharama kubwa kupeleka miradi ya umeme vijijini hivyo amewataka wananchi wa vijijini kuchangamkia fursa hiyo kwa kuutumia kwa shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa REA , Mhandisi Elineema Mkumbo, amesema hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imepanda kutoka asilimia 2 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 kufikia mwaka 2020. "Lengo letu ni kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote nchini vinapata umeme nyumba kwa nyumba.


Mhandisi Mkumbo ameeleza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vijijini inaenda sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji ambapo hadi sasa zaidi ya vitongoji 27,000 vimepatiwa umeme.


Post a Comment

Previous Post Next Post