Na Hadija Bagasha Tanga,
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema shule zinazojengwa na serikali kwa mpango wa kuboresha shule za sekondari nchini ziwe za mchepuo wa kilimo ili kuwasaidia vijana wanapomaliza elimu ya sekondari wawe wamejifunza nadharia ya kilimo.
Chongolo amesema shule hizo zitajengwa kila wilaya nchi nzima kwa lengo la kusogeza huduma ya elimu karibu na jamii.
Akizungumza wakati akikagua ujenzi wa shule ya sekondari inayojengwa kata ya Kisiwani wilayani humo, Chongolo alisema kuwa lengo lake ni kuwafanya vijana wanapomaliza elimu ya sekondari wawe na utaalamu wa kilimo.
"Chini ya mpango wa kuboresha elimu nchini shule za sekondari zinazojengwa nchini ziingizwe ziwe shule za mchepuo wa kilimo lengo vijana wakimaliza shule na utaalamu wa kulima kidogo kupata zaidi," alisema Chongolo.
Chongolo alisema shule hizo zaidi ya 200 zinazojengwa kwa fedha za serikali katika kila wilaya hapa nchini, zikifanywa za kilimo zitawafanya vijana kujua kile wanachokwenda kukifanya mra baada ya kumaliza masomo yao.
Alisema serikali imetoa uwamuzi wa kutoa elimu bila malipo ili kutanua wigo wa vijana kusoma na gharama zake kubebwa na serikali.
Katibu mkuu huyo aliwataka viongozi kuzisemea shule hizo zinazojengwa katika maeneo mbalimbali kwasababu ni jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan maono yake ameonelea ajenge shule hizo kwa ajili ya kusukuma mendeleo ya elimu.
"Serikali inajenga shule zaidi ya 200 katika kila wilaya hapa nchini kwa kutoa fedha nyingi, bahati mbaya watu hawazisemei na kuzionesha kama shule hizi zinajengwa na serikali," alisema.
Katibu mkuu alisema katika ziara yake anapita kuona ubora wa ujenzi, fedha zilizotolewa kama zimefika, matumizi yake na kama shule hizo zimejengwa katika eneo lenye uhitaji kama kusudio lake.
"Tumejiridhisha hapa muheza mmejenga kwa ajili ya kusogeza mbele maendeleo ya wananchi na mmewasogezea huduma hongereni sana," alisema Katibu Mkuu na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA.
Alisema atabeba agenda ya kwenda kumuomba Rais kiasi cha shilingi milioni 130 serikali iziwasilishe katika shule hizo ili ziweze kujengea mabweni kwa ajili ya wanafunzi, nyumba za walimu na kuongeza madarasa kwa ajili ya kidato cha tano na sita.
Awali mbunge wa muheza Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, alisema shule hiyo waliamua kuijenga katika kata ya Kisiwani kwasababu mbili muhimu ambazo ni watoto kutembea umbali mrefu kwenda Sekondari ya Shebomeza umbali wa kilometa 23.
"Mheshimiwa katibu mkuu ni mimi ndiyo hizi fedha za rais zaidi ya milioni 600 nilizileta hapa kimkakati kabisa kwasababu kwanza tuna hadithi ya watoto kutembea umbali wa kilometa 23 kwenda Sekondari ya Shebomeza kupata elimu, pia barabara ni changamoto," alisema.
Awali mkuu wa mkoa wa Tanga, Omari Mgumba aliendelea kumpongeza Rais kwa kusema kamba wilya ya muheza wanamuunga mkono kwa hatua yake ya kupandisha bei ya Mkonge hadi kufikia tani moja shilingi milioni 3.5 kutoka shilingi laki tatu na hamsini kwa tani.
Katibu huyo mkuu wa Chama cha Mapinduzi yupo mkoani Tanga kwenye ziara yake ya kichama ambapo amekutana na wananchi wa wilaya ya Lushoto ,Pangani na Muheza ,ziara ambayo pia itahusisha wilaya ya Tanga na wilaya ya Mkinga .
Tags:
HABARI