Mwenyekiti wa Taifa na Mwenyekiti wa bodi ya UMATI Sheikh Swed Twaibu Swed Akizungumza na Waandishi wa habari ( hawapo pichani) kuhusu vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo matukio yake yameripotiwa kuongezeka, Mkutano umefanyika katika ofisi za UMATI, Upanga Jijini Dar es salaam
Mkurugenzi wa idara ya fedha na Utawala , UMATI, Revocatus Kitteka ( wa kwanza kulia) na Meneja Rasilimali watu Elifuraha Matafu ( wa pili kushoto) wakimsikiliza Mwenyekiti wa UMATI ( hayupo pichani) wakati wa Mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 1, 2022
PICHA ZOTE NA YUSUPH DIGOSSI
*******************************************
Na Yusuph Digossi- Sauti za Mtaa Blog
Kufuatia kuongezeka kwa matukio mengi yanayoripotiwa na vyombo vya habari pamoja na vyombo vya dola hapa nchini kuhusiana na hali ya ukatili unaoendelea kutokea miongoni mwa jamii hasa ubakaji na ulawiti kwa watoto, Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) kimepinga na kulaani vikali vitendo wanavyofanyiwa watoto ambavyo vinaripotiwa kuongezeka hapa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mwenyekiti wa Taifa na Mwenyekiti wa bodi ya UMATI Sheikh Swed Twaibu Swed amesema kuwa vitendo hivo vimekua vikileta taharuki , wasiwasi, magonjwa na hata vifo kwa baadhi ya wahanga wa vitendo hivo.
Amesema vitendo vya ukatili sio tu vinaharibu na kukatisha ndoto za vijana wengi ambao hukata tamaa baada ya kufanyiwa vitendo hivo pia vinadhalilisha jamii ya Tanzania ambayo imekua ni mfano wa malezi bora ya watoto kwa muda mrefu.
" matokeo ya hali ya vitendo vya ukatili imewafanya vijana wengi kutofahamu wapi waende kuripoti mara tu wanapokutana na ukatili wa aina yoyote kwa kuwa mara nyingine ukatili unatokea ndani ya familia " Amesema Sheikh Swed
Kufuatia hali hiyo chama hicho kupitia Mwenyekiti wake kimetoa wito kwa Serikali kuhakikisha inasimamia maeneo yote muhimu hasa katika mambo ya kijamii kuanzia ngazi ya Kijiji hadi kata ambapo vitendo hivyo vinafanyika na Maafisa wa Ustawi wa Jamii na Maafisa Afya wako kila Kata.
Pia wameliomba jeshi la Polisi kupitia madawati maalumu kuwapokea kwa weledi waathirika ili wasipate wasiwasi wa kusambaa kwa habari hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania ( UMATI) , Suzana Mkanzabi amewataka Wazazi kujenga tabia ya kujenga urafiki na vijana wao na kuzungumza nao kila wakati badala ya kuwa na dhana ya kuwa watoto wao hawajui chochote.
Ameongeza kuwa ili kuondokana na changamoto hizo UMATI kwa kushirikiana na wadau wengine inaratibu afua zinazowawezesha vijana balehe, Wanawake walio kwenye ndoa na watu wanaoishi na ulemavu kutambua haki zao na kutovumilia viashiria vya ukatili wa aina yoyote na kuripoti kwenye mamlaka husika kama dawati la Jinsia au uongozi wa Kijiji.
Tags:
HABARI