TUICO YAIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA MCHAKATO MISHAHARA SEKTA BINAFSI.





Na Mwandishi wetu

Juni 10, 2022 - Morogoro.

Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimeiomba Serikali kuharakisha mchakato wa nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.

Akizungumza katika Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la TUICO kilichofanyika mjini Morogoro, Mwenyekiti wa Taifa wa TUICO ndugu Paul Sangeze amesema ni takribani miaka nane sasa kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi hakijaongezwa.


“Nimuombe waziri mwenye dhamana kuangalia kwa haraka suala la kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ili wakati watumishi wa umma watakapoongezewa, basi na watumishi wa sekta binafsi nao waongezewe,” amesema ndugu Sangeze.

Wakati huo huo, Chama cha Wafanyakazi TUICO kimeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3. TUICO kimesema nyongeza hiyo itaongeza morali ya wafanyakazi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. 

“Kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ongezeko hilo la mshahara. TUICO tunaahidi kumuunga mkono katika uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi hapa nchini,” amesema ndugu Sangeze.


Pia, Chama cha Wafanyakazi TUICO kimeipongeza serikali ya Tanzania kwa kuja na kanuni mpya ya mafao ya pensheni inayopandisha kiwango cha kikokotoo kutoka asilimia 25 hadi 33 hali ambayo itaimarisha uhakika wa mafao ya wafanyakazi na wanachama wanaostaafu.

“Nimshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuja na kanuni ya pamoja ya asilimia 33 kwa suala la kikotoo. Kukamilika kwa suala la kikotoo kunawapa wafanyakazi uhakika wa mafao yao baada ya kustaafu,” amesema ndugu Sangeze.


TUICO kimewasihi wafanyakazi nchini kujiunga na Chama hicho kwani kinapofunga Mikataba ya Hali Bora za Kazi vipengele kama malipo, nyongeza ya mishahara, posho, saa za kazi, likizo, mapumziko na sikukuu, afya na usalama sehemu za kazi, mafao ya uzeeni, upunguzwaji na suala la uzazi huzingatiwa.

Kwa mwaka 2021 pekee mikataba ya pamoja takribani 80 ikiwa ni pamoja na Mikataba ya Hali Bora za Kazi imefungwa baina ya Chama cha Wafanyakazi TUICO na maeneo mbalimbali hapa nchini huku mashauri na migogoro ya kikazi zaidi ya 1,400 imesimamiwa na Chama hicho katika ngazi za na kwa ana, Tume ya Usuluhishi na Maamuzi (CMA) na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.



Post a Comment

Previous Post Next Post