Dar es Salaam
Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) leo Jumamosi, Machi 05 mwaka 2022 kimefanya Matendo ya Huruma katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutoa misaada hiyo ikiwa ni pamoja na viti vyenye magurudumu, mashine za kupimia presha na kadhalika, Mwenyekiti Kamati ya Wanawake TUICO Mkoa wa Temeke Bi. Magdalena Lucas Samkumbi amesema wameamua kuungana na wanawake wengine duniani kusherehekea nafasi ya mwanamke katika jamii ikiwa ni Mwezi wenye Siku ya Wanawake Duniani.
“Tumekuja hapa Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kutoa zawadi kutokana na hii siku ya Wanawake Duniani. Tumekuja kuleta vifaa kwa ajili ya hospitali na kwa ajili ya wagonjwa. Tumeleta wheel-chairs [viti vyenye magurudumu], mashine za kupimia presha. Tumeona hii siku tuitumie kwa namna hiyo ikiwa ni moja ya njia za kukitangaza Chama,”
“Wafanyakazi tupo na tunawatetea na katika huduma za kijamii tupo. Huu ni mwendelezo na tunategemea wakati mwingine tutakuwa sehemu nyingine. Kila mwaka tunakuwa na tukio maalumu,” alisema Bi. Samkumbi
Kwa upande wake Bi. Juhudi Nyamboka, Afisa Afya Hospitali ya Rufaa ya Temeke amekishukuru Chama cha Wafanyakazi TUICO na kutoa rai kwa wadau wengine kuendelea kufanya hivyo.
“Kwa tukio hili kupitia Chama cha Wafanyakazi TUICO, tunashukuru sana. Wamekuja kutufariji sisi na wagonjwa. Kama watoa huduma tunapoona wadau wengine wanakuja huwa tunafarijika, kwa sababu wanakuwa wametupunguzia [majukumu kwa] sehemu kubwa.”
“Pia nitoe hamasa hii kwa taasisi, mashirika na wadau wengine kujali matendo ya huruma hasa kwenye maeneo yenye uhitaji kama hospitali na magereza. Lakini pia nitoe wito wa kuhitaji damu, tuna shida ya damu katika hospitali zote karibia,” amesema Bi. Nyamboka