Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar akemea udhalilishaji wa kijinsia wa wanawake na watoto Nchini.



Na Hadija Bagasha Tanga, 

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulah amesema bado kuna tatizo la udhalilishaji wa wanawake na watoto kwenye Mikoa mbalimbali Nchini jambo linalohitaji kukemewa na kila mwana jamii.

Pia Makamu wa pili wa Rais amekitaka chama cha mapinduzi Mkoa wa Tanga kutowavumilia watendaji wazembe wa serikali ambao watakuwa ndio chanzo kikuu cha kukichafua chama cha mapinduzi CCM. 


Makamu wa pili wa Rais ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kichama Mkoani Tanga ambapo amewaomba viongozi wote wa chama cha mapinduzi CCM kuhakikisha kwenye maeneo yao wanasimama kwenye misimamo ya pamoja ya kupambana na vitendo hivyo. 

Aidha amesema kuwa jamii inaweza kuishi bila udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto kama kila mmoja atatimiza wajibu wake ili kuweza kuondokana na matukio hayo. 


"Kwenye mikoa yetu hii bado kuna changamoto ya udhalilishaji wa wanawake na, watoto kwa maana ya udhalilishaji wa kijinsia bado vijana wanaendelea kudhalilishwa bado vijana wanaendelea kudhalilishwa bado kina mama wanaendelea kudhalilishwa naomba nichukue nafasi hii kuwaomba viongozi wote wa chama cha mapinduzi sote tuko hapa kwenye maeneo yetu waheshimiwa wakuu wa wilaya, wakuu wa Mikoa,  viongozi kwa maana wenyeviti wa wilaya,  madiwani wetu,  wabunge,  wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wetu wote tuhakikishe sotw tunasimama kwenye muelekeo mmoja wa kupinga udhalilishaji, "alisisitiza Abdulla. 


Sanjari na hayo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amekiasa chama cha mapinduzi ccm Mkoa Tanga kuhakikisha kinawashughulikia watendaji wote wazembe wanaotumika kukichafua chama hicho na kuwataka viongozi mbalimbali kuwaeleza wananchi maendeleo yanayofanywa na serikali yao. 

"Sambamba na hilo kuna utumiaji wa dawa za kulevya tumepakana na maeneo mengi Tanga na maeneo mengine bado tuna changamoto ya dawa za kulevya haya mambo lazima ndugu zangu tuweke kipaumbele cha kuyaondosha, "alibainisha Abdulla. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba ameelezea utejelezaji wa miradi ya maendeleo na kiasi cha fedha ambacho serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kwenye Mkoa huo ikiwemo maboresho ya upanuzi wa kina katika bandari ya Tanga.  


"Tunaendelea kumshukuru Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa nia yake njema ya kuifungua Tanga kiuchumi na kuirudisha Tanga ya Viwanda kama pale mwanzo moja amefanya mradi wa kimkakati anafanya maboresho makubwa ya bandari yetu ya Tanga ameleta na nimepokea zaidi ya bilioni 429 kwajili ya upanuzi wa bandari ya Tanga na utekelezaji wake tumefikia, asilimia 90 na mkandarasi anatakiwa kukabidhi kazi mwezi wa 3 kesho kutwa, "alisema Mgumba 

Naye Mwenyekiti wa ccm Mkoa Tanga Rajab Abdulrahman amesema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinafanya vizuri kwenye chaguzi mbalimbali zijazo. 


"Tunaposema tumedhamiria kwenye uchaguzi wa mwaka 2024 mwakani wa serikali za mitaa kwenye vijiji pamoja na vitongoji kwamba hatutobakisha kitongoji hata kimoja,  vijiji hata kimoja na hata mtaa pia vyote vitakuwa chini ya chama cha mapinduzi tunaposema hayo huwa tunakuwa tumemaanisha, "alisisitiza Mwenyekiti Rajab. 

Makamu wa pili wa Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na mlezi wa chama cha mapinduzi ccm yupo ziarani Mkoani Tanga kwa sita ambapo pamoja na mambo mengine atafanya mikutano ya hadhara pamoja na mikutano ya ndani ya chama hicho. 




Post a Comment

Previous Post Next Post