OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki amesema kipindi cha mwezi Julai - Disemba 2022 kwa mwaka wa fedha 2022/23 Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi Bilioni 485.42 sawa na asilimia 48 ya lengo la mwaka na asilimia 96 ya lengo la nusu mwaka.
Ameeleza hayo leo tarehe 27 januari 2023 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya ukusanyaji wa Mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/23 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Waziri Kairuki amesema katika makusanyo hayo, Mapato yasiyolindwa ni shilingi bilioni 396.67 na Mapato lindwa ni shilingi bilioni 88.73
Waziri Kairuki amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.02 kutoka kwenye vyanzo vyake Vya ndani.
Aidha, Waziri Kairuki amesema makisio ya mapato ya ndani yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 863.90 mwaka 2021/22 hadi Shilingi Trilioni 1.012 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 17 ambapo ni ongezeko la Shilingi Bilioni 148.
Amesema mafanikio hayo yametokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuimarisha usimamizi wa mfumo wa kukusanyia mapato wa TAUSI, matumizi ya mashine za kukusanyia mapato (POS), msisitizo unaotolewa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia vyombo vya habari na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kiutumishi.
Kadhalika, amesema Halmashauri zimetumia Shilingi bilioni 132.38 kutekeleza miradi ya maendeleo na Shilingi bilioni 160.96 zimetumika kwa matumizi ya kawaida ya mapato halisi yasiyolindwa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2022.
Waziri Kairuki amesema Halmashauri zimechangia Shilingi bilioni 28.48 kwa ajili ya mikopo ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika kipindi cha Julai - Disemba, 2022.
Tags:
HABARI