Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akiwa katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Samora, Iringa Mjini; Amesema Kesho tarehe 13 Agosti, 2022 Wizara ya Kilimo, itatangaza majina ya Mawakala na utaratibu mzima wa namna ya kujisajiri ili Wakulima walio mijini na vijijini iwe rahisi kununua mbolea ya ruzuku sawa sawa na lengo la Serikali.
Waziri Bashe amesema kesho Jumamosi, Wizara kupitia vyombo mbalimbali vya habari, itatangaza majina ya Mawakala, mikoa na wilaya, vitongoji na vijiji walipo pamoja na utaratibu wote wa namna ya kujisajili ili kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa mbolea ya ruzuku, ifikiapo tarehe 15 Agosti, 2022 hatmae kufikia lengo la Serikali la kumsaidia Mkulima kupunguza makali ya bei ya mbolea.
Waziri Bashe ameongeza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 150 zilizotengwa kwa pembejeo ni kwa ajili ya Wakulima wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kumbagua yeyote, mwenye eneo dogo au kubwa.
Waziri Bashe amewakumbusha Wakulima kuhusu bei za mbolea kama ifuatavyo: -
“Bei ya mbolea ya kupandia aina ya DAP ambayo awali ikuwa ikiuzwa kwa shilingi 140,000 sasa itauzwa kwa shilingi 70,000; Mbolea ya kukuzia aina ya UREA ambayo ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi 150,000 sasa itauzwa kwa shilingi 70,000; Mbolea ya CAN ambayo awali ikuwa ikiuzwa hadi shilingi 120,000 sasa itauzwa kwa shilingi 60,000.” Amekaririwa Waziri Bashe.
Waziri Bashe ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha Wakulima kuwa Serikali ya Awamu ya Sita tangu imeingia madarakani imekuwa ikitoa fedha nyingi kwenye eneo la kugharamia pembejeo.
Waziri Bashe amesema awali Seriklai ya Awamu ya Sita ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 91 kwa ajili ya ununuzi wa viuatilifu (Dawa aina ya Salfa) kwenye zao la korosho pia ilitoa zaidi ya bilioni 60 kwa ajili ya kununua viuatilifu kwenye zao la pamba.
Tags:
HABARI