Na Yusuph Digossi- Sauti za Mtaa Blog
Katika kuongeza ufanisi kwa wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi na matibabu ya wagonjwa mahututi Taasisi ya mifupa Moi kwa kushirikiana na Chuo cha Sayansi Shirikishi Cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MUHAS) wamezindua maabara ya mafunzo kwa wataalamu wa kada ya dawa za usingizi na ganzi ambayo imeripotiwa kuwa itapunguza uwezekano mkubwa wa kumuweka mgonjwa katika hatari ya kupoteza maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa maabara hiyo uliofanyia katika Taasisi ya Mifupa Moi leo Jumatatu , Mei 16 Prof. Charles Mkonyi, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini MOI , ambaye alikua Mgeni Rasmi katika hafla hiyo amesema kuwa maabara hiyo inatoa fursa ya kufundisha katika mazingira ambayo mtaalamu akifanya kosa inakuwa rahisi kurekebisha hivyo itapunguza madhara ya moja kwa moja anayoweza kupata mgonjwa kutokana na makosa hayo.
Ameongeza kuwa hatua ya uzinduzi wa mradi huo inachagizwa na kasi na maendeleo ya Sayansi na Teknlojia ambayo yanapunguza uwezekano mkubwa wa kumuweka mgonjwa katika hatari ya kupoteza maisha.
Pia amesema kuwa maabara hiyo inaweza kutumika na watu ambao ni wataalamu kwaajili ya kuendeleza na kunoa stadi ili kuongeza ufanisi wao ambao utaendelea kuokoa maisha ya watanzania.
Kwa upande wake Dkt. Pascal Joseph, Kaimu Mshauri wa wanafunzi chuo cha MUHAS akimuwakilisha makamu Mkuu wa chuo amesema kuwa uzinduzi wa maabara hiyo ya mafunzo ya dawa za usingizi pamoja na matibabu mahututi itasaidia kupunguza uhaba wa Rasilimali watu katika matibabu ya magonjwa mahututi kwakuwa idadi ya wataalamu hao bado ipo chini hapa nchini.
"Rasilimali watu katika matibabu ya usingizi na magonjwa mahututi Bado iko chini Sana hivyo kwa kuliona Hilo tulianzisha mitaala tofauti ya madaktari wauguzi kwaajili ya mafunzo ya Shahada ya kwanza na Shahada ya Uzamili" Amesema Dkt. Pascal
Naye Edwin Lugazia, Mkuu wa idara ya usingizi na Ganzi amesema mradi huo lengo la kutengeneza walimu ambao watawafundisha watu wanaotoa dawa za usingizi na ganzi ambao watafikia viwango vinavyohitajika kimataifa kwa umahiri, kujenga maabara ambazo zitatumika kufundishia mwanafunzi akafanya mazoezi bila kufanya mazoezi kwa mgonjwa.
"Maabara inasaidia kufundisha umahiri kwenye kitendo chenyewe ambapo mwanafunzi akienda kumpatia huduma mgonjwa anakuwa kashafahamu nini Cha kufanya na kujua wapi anahitaji usaidizi" Amesema Lugazia
Amesema wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi wapo 75 nchi nzima, na tulisema wataalamu wanatakiwa 25 lakini hapa wapo wengi lakini wamegawanyika katika vipengele mbalimbali.
Tags:
HABARI